Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Sayyid Ali Fadlullah, Imam wa Swala ya Ijumaa Beirut na mwanazuoni wa Kishia wa Lebanon, alifanya kikao cha mazungumzo katika Kituo cha Utamaduni wa Kiislamu kwa anuani “Mwezi wa Ramadhani na Kuimarisha Kipengele cha Kibinadamu”, ambapo alijibu maswali na mitazamo kuhusu maendeleo ya hivi karibuni nchini Lebanon na katika eneo zima.
Hujjatul-Islam Fadlullah mwanzoni mwa kikao alisisitiza kwamba, jambo muhimu zaidi aliloweka Mwenyezi Mungu katika mwezi huu ni faradhi ya saumu; faradhi inayotualika kuvumilia ugumu wake kwa subira na kwa nia ya kimungu. Hata hivyo, swali ni kwa nini kumekuwa na msisitizo mkubwa juu ya saumu, na ni ipi siri ya kupewa umuhimu maalumu kwa wafungaji? Je, ni kuacha kula, kunywa na vitu vingine vinavyobatilisha saumu tu, au kuna malengo na makusudio ya kina zaidi yaliyofichika nyuma ya faradhi hii?
Aliongeza: Hadithi zimeeleza wazi kwamba lengo la saumu ni kuamsha hisia za kibinadamu, kiroho na kimaadili ndani ya mwanadamu; kwamba mtu aelewe dhiki za watu na matatizo yao, na ahisi uchungu wa njaa ya maskini na mateso yao. Utajiri unaweza kumfanya mtu asitambue uhalisia wa mateso ya wengine, kwa kuwa hudhani kwamba kila mtu anaishi kama yeye. Kwa hiyo, faradhi ya saumu imekuja kuhuisha ndani ya nyoyo hisia ya uwajibikaji kwa wahitaji, na kuanzisha uhusiano kati ya swaumu na kuwasaidia wanyonge.
Imam wa Ijumaa wa Beirut aliendelea: Leo kuliko wakati mwingine wowote tunahitaji kuimarisha hisia ya uwajibikaji kwa wale walioko katika dhiki za maisha, na tunapaswa kujikomboa na ubinafsi; ubinafsi unaomlazimisha mtu kufikiria tu mahitaji yake hata kwa gharama ya kuwadhuru wengine, na unaolisha roho ya tamaa na uhifadhi wa bidhaa bila kuzingatia athari zake kwa wanyonge. Mageuzi haya ya kiroho yanaweza kusaidia katika kukabiliana na hali ngumu za kiuchumi na kimaisha; ambapo maskini wanazidi kuwa maskini na matajiri wanazidi kuwa matajiri, na suluhisho pekee ni mshikamano wa kweli. Licha ya umuhimu wa juhudi za mtu mmoja mmoja, msingi wa kazi uko katika kuimarisha juhudi za pamoja na zilizopangwa.
Alisisitiza umuhimu wa kukumbuka daima kwamba Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kula kidogo si wa kula kupita kiasi; mwezi wa kunufaika na wakati si wa kuupoteza; mwezi wa utulivu si wa hasira; mwezi wa kufungua nyoyo na kuwasiliana si wa kujitenga na kujifungia.
Hujjatul-Islam Fadlullah alisema: Heri kwa wafungaji ambao si tu wanaacha kula na kunywa, bali pia hujiepusha na kila lililo haramu; heri wale wanaoufanya Mwezi wa Ramadhani kuwa uwanja wa kufikia radhi na mapenzi ya Mwenyezi Mungu; na heri wale wanaofikiria tangu mwanzo wa mwezi jinsi watakavyotoka katika Ramadhani wakiwa wamejikusanyia akiba iliyojaa kwa ajili ya dunia na Akhera yao.
Akijibu swali kuhusu kuthibitisha mwanzo wa mwezi wa hijria, alifafanua: Uthibitisho wa mwanzo wa miezi ya hijria si jambo jipya linalohitaji kurejea kwa Marji' aliye hai; mukallaf anaweza kubaki juu ya fatwa ya Marji' aliyefariki ambaye bado anamfuata katika taqlidi, kama ilivyo katika masuala mengine ya fiqhi. Huu ni utaratibu unaojulikana katika fiqhi ya Kishia kwa Maraji' waliokwishafariki ambao wafuasi wao wanaendelea kuwafuata.
Imam wa Ijumaa wa Beirut aliongeza kuwa, jukumu la sasa katika suala hili ni kutekeleza tu rai ya kifiqhi iliyokubaliwa kutoka kwa Maraji' muhtaramu, baada ya kurejea katika vituo sahihi vya uangalizi wa kielimu ambavyo kila mukallaf anaweza kuvirejea mwenyewe; kwa sababu suala hili halihitaji kutoa hukumu mpya, bali linategemea msingi thabiti wa kifiqhi.
Hujjatul-Islam Fadlullah alilaani vikali mashambulizi ya mara kwa mara ya utawala wa Kizayuni dhidi ya kusini na eneo la Biqa’ nchini Lebanon, na akaitaka serikali kutumia uwezo wake wote katika nyanja zote kukabiliana na mashambulizi haya, na kutolifungia suala hilo katika mjadala wa “ukiritimba wa silaha” pekee; kwa kuwa adui huyu ana malengo yanayozidi hilo na hatoi aina yoyote ya mapendeleo. Aidha alitoa wito wa kuharakishwa kwa utekelezaji wa ahadi za serikali kwa wananchi wa Lebanon, ikiwemo kuandaa mkakati wa kina wa usalama wa taifa kwa ajili ya kulinda mamlaka ya nchi na rasilimali zake, na kuwatetea wananchi dhidi ya mashambulizi haya endelevu.
Mwanazuoni huyu wa Kishia alionesha mshangao wake kwa msisitizo wa serikali juu ya maamuzi yasiyo sahihi ya kodi, akisema: Serikali inajiita “serikali ya mageuzi na uokozi”, ilhali kivitendo ni serikali ya kutoza kodi bila kuchunguza madhara yake ya kijamii na kibinadamu; maamuzi ambayo huenda yakasababisha mlipuko wa kijamii.
Hujjatul-Islam Fadlullah, akionya juu ya matokeo ya maamuzi hayo, aliongeza: Sauti ya upinzani inapaswa kuinuliwa, kwa kuwa hatua hizi zinatishia usalama wa kijamii na huenda zikapendelea maslahi ya tabaka fulani juu ya wengine. Kupinga sera hizi kunatokana na uchungu kwa ajili ya taifa; upungufu wa bajeti haupaswi kujazwa kutoka mifukoni mwa maskini, bali inapaswa kushughulikiwa kupitia mpango wa kina wa mageuzi ya kifedha, kurekebisha mfumo wa kodi, kupambana na upotevu wa rasilimali, kurejesha haki za serikali katika mali za baharini, kupunguza matumizi na kuimarisha mapato ya umma ili kufikia uadilifu na uthabiti.
Mwisho, alizitaka taasisi za uangalizi na Shirika la Kuwalinda watumiaji kuchukua hatua za haraka kudhibiti ongezeko lisilodhibitiwa la bei na wimbi la gharama katika masoko, ili kuwalinda wananchi na usalama wa kijamii.
Maoni yako